Ruka hadi kwenye maudhui makuu

Pata muda wa utulivu(Take time to be quite)

Habari za asubuhi mpendwa msomaji wa Makala za kila siku zijulikanazo kwa jina la Wazo La Leo.
Leo nakwenda kuongelea PATA MUDA WA UTULIVU (TAKE TIME TO BE QUITE).
Katika dunia hii tuliopo michaka michaka au kwa lugha nyepesi na kueleweka kwa walio wengi namaanisha ubize umetufikisha mahali tunashindwa kuwa na muda wa kutosha kutulia katika hali iliyojaa utulivu,
Kinachoendelea katika maisha yetu ni kukimbizana, kukimbizana huku tukiwa tunasikilizishwa makelele yanayotuzunguka, mara siasa, mara ajali, mara raisi kasema lile, mara yanga na simba, mara Mugabe, basi ili mradi tunasikilizishwa kila kitu pasi kuchuja. Hii ni hatari kwa mstakabali wa maisha yetu.
Kitu ninachotaka kukisema leo ni kwamba hatutakiwi kukubaliana na maisha yasiyo na uhalisia kwa mgongo wa kukimbizana kusiko na tija ya aina yoyote. Kila mtu bize na ukifatilia kinachomfanya mtu kuwa bize, utagundua ni ubize wa kumfananisha na mtu anayetengeneza pesa kwa kasi ya ajabu, lakini kumbe ni ubize wa kutengeneza madeni na matatizo kadha kwa kadha. Mungu tusaidie.
Ninachokiomba kwako kuanzia leo, kila wakati uwe na swali mdomoni la kujiuliza wewe mwenyewe, niko bize nikifanya nini? Tulizana na jipe jibu sahihi. Kwa lugha nyepesi ni kwamba hayo yanayokushughulisha ndiyo yanayokupeleka kwenye malengo yako ya kimaisha? Je hayo uyafanyayo mwisho wa siku yatakupa nyumba ya ndoto yako, gari la ndoto yako, kuwa na shirika la kutoa msaada kwa watu waishio katika mazingira magumu na kadhalika. Mimi sijui una ndoto gani, nimejaribu kutoa mifano tu ili ikuwezeshe na wewe kuainisha malengo yako na kuona kama shughuli uzifanyazo na kukukosesha muda, je zinakukimbiza kufikia malengo yako? Ni muhimu sana uwe ukijiuliza hili swali huenda ukasaidika.
Ukiona majibu uyapatayo juu ya yale yanayokufanya uwe bize hayana mbele wa nyuma kwa maana hayakupeleki kwenye ndoto zako, huhitaji mwalimu Seth Simon Mwakitalu akuambie anza kuachana na hizo shughuli. Ziko shughuli nyingi zimewalevya watu utafikiri ni mithili ya mateja. Mfano upenzi wa mpira uliopitiliza. Mimi ni muumini kwa kuwa na kiasi. Wengi wetu hatuna kiasi. Unakuta mtu mpaka anaugua au anashindwa kula au anapoteza siku bila kuzalisha ati tu timu yake imefungwa. Ama kweli mapunguani wako wengi. Ukienda kuangalia kwenye regista ya timu ya mpira ili kujiridhisha kama ana hisa utashangaa hata kadi ya uanachama hana. Du Mungu tusaidie. Na mengine mengi tusaidiane kuorodhesha.
Ukianza kujitenga na shughuli zote zisizo na tija, basi wewe sasa unaelekea kwenye ukomavu wa kifikra, maana wengi wana nywele zilizo na majivu lakini kifikra ni sawa na mtoto aliyezaliwa leo kwani kila ukimshauri aache kufanya upuuzi hata aelewi. Sasa ndio natambua kwa nini wahenga walisema mtoto akichezea wembe mwache umkate siku nyingine hatorudia. Hivyo ukifanikiwa kuachana na shughuli zisizo na tija basi anza kupata muda wa utulivu
Moyo wa mwanadamu ulivyoumbika ni kwamba unahitaji muda wa utulivu ili kukupa mrejesho wa yaliyopita. Hapa namaanisha mioyo tuliyo nayo inatuhitaji tufike mahala tujifanyie tathmini ya maisha tunayokwenda nayo. Tathmini hii hufanyika kwa ubora wa hali ya juu tunapokuwa na muda wa utulivu (Times of quiet reflection). Hii hutusaidia kujichimba ndani kabisa na kuibuka na mawazo (Ideas) yatakayo tusaidia kuboresha maisha yetu ya baadae. Tukifanikiwa kufanya hivi, mioyo yetu huwa huru kuanza kutupeleka kwenye muelekeo sahihi kufikia malengo yrtu.
Sasa nisemeje? ANZA KUPANGILIA MUDA WA KUKAA KATIKA HALI YA UTULIVU, muda ambao mimi nauita ni muda wa malengo (Dream Time). Nitafurahi kama utaanza mara moja kuanzia leo kupangilia muda wa utulivu. Ninaposema muda wa utulivu namaanisha mahali pasipo na simu ya aina yoyote ile. Ushauri wangu zima simu na acha nyumbani maana wewe si tephone operator bali ni ulimbukeni tu kila saa na simu utafikiri teja lisilojitambua. Hebu dhibiti simu yako na siyo simu kukudhibiti wewe. Eneo ambalo halina mtu wa aina yoyote hata mpenzi wako, maana siku hizi tumetekwa na utamaduni wa magharibi kila mtu baby wangu mara sweet heart na upuuzi kibao. Angalia usije juta maishani hivyo sivyo, tumeiga utamaduni wa wenzetu. Mungu tusaidie. Tena hata computer isiwepo katika eneo utakalokuwa umekaa kwa utulivu. Kimsingi uwe na peni, noti book pamoja na mawazo yako.
Anza kufikiria mambo yakufanyao kusisimuka na kuhamasika. Unapokuwa katika hali ya utulivu anza kufikiria mambo yasababishyo damu yako kwenda mbio. Hebu kumbuka utotoni ulipokuwa ukiulizwa ukiwa mkubwa utafanya nini?. Wengi walisema nitakujengea nyumba baba, nitakununulia gari na utakuwa pilot na mengine mengi. Natamani mtu angekurekodi maana sehemu kubwa ya hayo ndio ndoto zako zilizosheheni moyoni. Lakini tujiulize umefanya nini?. Ni aibu maana hata baskeli hujaweza kununua. Hivi tunaishi au tuna pumua pumua tu kisha tujiishie.
Kitu gani ungependa kukifanya? Yaani iwe cha kukufurahisha au kwa ajili ya kupata ridhiki ya maisha. Nini ungependa kukamilisha katika maisha? Hebu niorodheshee vitu vyote ambavyo ungependa kuvikamilisha iwapo pesa si tatizo kabisa. Hebu kuwa mkweli wa nafsi yako. Orodhesha bila kuogopa maana pesa si tatizo tena. Je ni orodha gani unaipata ambayo ungeweza kamilisha hapa duniani iwapo pesa si shida tena.Ukiweza kujibu haya maswali, utajisikia kushangazwa na ukubwa wa mambo uwezayo kuyafanya kwa kuhakikishiwa tu mafanikio na kwamba pesa si tatizo kwa kuwa upo kwenye ukanda wa ndoto zako (Dream Zone). Hebu itafakari hiyo orodha. Hayo ndio mambo uliyoitiwa duniani kukamilisha. Sasa pitia orodha hiyo na uone ni kipi umetekeleza?
Muda wangu unanitupa mkono, lakini niseme hivi: Ni mpaka pale tutakapo weza kuwa na ratiba ya utulivu ndipo kwa hakika tutatambua na kuanza onja radha ya ndoto zetu.
Ni mimi mwalimu wako Seth Simon Mwakitalu 0754 441 325/0714 051 155/0788 493 836 au barua pepe ssmwakitalu2013@gmail.com tukutane tena kesho Mungu akipenda.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Akili Hisia (emotional intelligence).

Lea mtizamo wa kisayansi, akili hisia ni ule uwezo wa mtu kuweza kutawala anachokiona kwenye mazingira aliyomo. Hii inaamanisha kwamba aweze kutawala mazingira kwa kutumia akili ya hisia zake na wale waliomzunguka. Mtu atawezaje kuelewa kwa kutumia hisia, ishara zinazoonekana kwenye mahusiano mbalimbali bila kuambiwa sentensi au hata neno moja? Utawezaje kutawala hisia zako na za watu wengine katika mazingira uliyomo? Kuna hatua sita za kuchukua ili akili hisia zako zikupe mafanikio unayoyatafuta. #1. Hatua ya kwanza ni wewe mwenyewe kujitambua. Kujitambua ni kitu muhimu kabisa linapokuja suala la akili hisia au emotional intelligence (EQ). Hebu tujiulize ni kwanini? Bila akili hisia hatuna namna yeyote ya kujitathmini kwa vile vipaji ama tulivyo navyo, tusivyo navyo au tunavyohitaji kujifunza ili tuweze kufanikiwa katika mambo yetu mbalimbali. Utaishia kuwa kama kipofu, maana hutaona chochote katika mazingira yaliyokuzunguka. Utapata shida kubwa kutumia mikono isiyoonekana. Aki...

Timiza Malengo Yako na Joel Nanauka.

Ninamshukuru Mungu sana kuweza kuwa na waandishi mashuhuri wa kitanzania ambao wanaweza andika vitabu kwa lugha ya Kiswahili na kusaidia watanzania wengi zaidi. Kitabu cha Timiza Malengo ni kitabu cha aina yake na kamwe si cha kukosekana kwenye maktaba yako. Kama kuna kitu familia yako inabidi ikushukuru basi ni hichi kitabu. Mimi ni msomaji sana wa vitabu na niseme tu ukweli kitabu hichi ni hazina tosha na hakikisha unapata nakala yako. Wahenga walisema tusiandikie wino wakati mate yapo. Nilichokifanya ni kukupatia sehemu ya hichi kitabu kutoka ukurasa wa 29 hadi 40 neno kwa neon ujisomee na useme mwenyewe je uko tayari kukikosa hichi kitabu? Tafadhali fuatana name nikinukuu kitabu cha Joel Nanauka kwa idhini yake kama ifuatavyo:- NJIA MBILI ZA KUTAMBUA KUSUDI LA MAISHA YAKO: Siku moja wakati Tiger Woods anahojiwa na mtangazaji akamwabia ‘’It seems like you like golf so much’’ (Inaonekana kuwa unaipenda gofu sana).Tiger Woods akamjibu, ‘’Not only I like golf but I am golf,’’ a...

CONSCIOUS NA SUB-CONCIOUS MIND

Wazo La Leo Hongera sana mwanakarakana ya ubongo kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana. Leo nimeona vyema nizungumzie maana ya maneno ambayo tumekuwa tukiyasikia mara kwa mara. Conscious na Subconscious. Kwanza unatakiwa uelewe "sub" maana yake nn, hii ni prefix...ikiwa na maana ya "below" something, sio negative or opposite that something. Kwa hiyo maana ya "conscious mind" ni kujitambua na subconscious mind means: internal sense of being ambayo consious mind haiwezi decipher, i mean kukupa maono halisi, wakristo wanaita nafsi, mfano mzuri wa activities za subconscious mind ni ndoto Conscious mind-ni kutumia akili wakati tendo fulani linafanyika. Hii inatokea pale mtu anapokuwa hana uzoefu wakati anafanya jambo/tendo fulani, kutokana na kutokuwa na uzoefu inabidi atumie uzingativu wakati wa kutekeleza jambo/tendo husika. kwa mfano mtu anayej...