- MTU ANAYECHEZEA MUDA = MTU ANACHEZEA PESA
- MTU ANAYECHEZEA PESA = MTU ANACHEZEA HATIMA YAKE KAA MBALI NA MTU HUYU NI SUMU KULIKO KANSA.
Jambo la kwanza nitaongelea kuhusiana na utafiti uliofanyika na kuonesha ya kuwa angalau kila familia kuna mtu mmoja ambaye akikujia na kukusomesha lazima utatoa pesa, sijui niwaite matapeli bado nazidi kutafuta lugha nzuri nataabika lakini nisaidie kuwapatia jina sahihi.
Ninachojaribu kuelezea hapa ni kwamba kuna watu hapa duniani ni wabunifu wa kutunga stori ili kujipatia pesa. Watu wa jinsi hii usiombe kukutana nao maana ukimpa tu nafasi akajieleza lazima utatoa pesa.
Inawezekana kabisa ukajisemea ya kwamba fulani akija kwangu simpi hata senti tano. Kinachoshangaza kwa ubunifu maridhawa walionao utajikuta si tu nunampatia pesa bali pia unamsaidia kumtafutia na kwa wengine wamuongezee.
Sijui kama ninachongea umekutana nacho maishani au unawafahamu watu wa jinsi hiyo katika jamii zetu kama sio kwenye familia zetu.
Yawezekana kabisa wengine wamo katika kundi hili. Kama umo humu ndani basi mshukuru sana Mungu maana siku ya ukombozi imewadia.
Imegundulika pasi shaka ya aina yoyote ya kuwa watu wote walio wabunifu kutunga stori za kujipatia pesa wamekosa mtu wa kuwasaidia kutwisti ubunifu huo kuelekeza kwenye ubunifu wa kujitengenezea pesa kama njugu.
Ukweli ni kwamba watu wa jinsi hii wana uwezo mzuri sana wa kubuni kitu kikatokea isipokuwa sasa wameelekeza ubunifu wao kwenye sehemu hasi. Ubunifu huo huo ukielekezwa kwenye kutengeneza pesa, kubuni miradi na kadhalika watatajirika sana.
Jambo la pili – Matajiri wote wanapigania wasipoteze muda, wakati masikini wote msimamo wao ni kupigania pesa isipotee.
Ndio maana mtu yuko radhi akae sehemu chafu yenye mainzi aweze kula chakula cha bei rahisi yaani mfano sahani sh. 500. Hapa anahurumia pesa yake isipotee maana ndicho kilichojengeka kwenye ubongo hata kama uwezo wa kula sahani ya 1,500 anao.
Mtu wa jinsi hii hata akiwa na mafanikio ni ngumu sana kubadilika kwa sababu ya Imani iliyojengeka kwa muda mrefu jinsi ya kuichukulia pesa tangu akiwa mdogo, akitumwa anaambia angalia kitu cha bei rahisi. Mpaka mtu anazeeka anajikuta amejengeka kiimani ya kwamba ni vyema kuihurumia pesa. Badala ya kutumia pesa kutokana jinsi ilivyo.
Pesa kimsingi ni mtumishi. Ndio maana haitanichukua muda kutoa uamuzi pale jirani anapokuwa na mgonjwa na hana pesa ya taxi. Nitawapatia mtumishi wangu pesa awasaidie maana hiyo ndio kazi yake na pia kitendo hicho kinanihakikishia mimi kuendelea kuwa na pesa Zaidi. Maana kutoa ni bora kuliko kupokea.
Naomba nikupe mfano ili kulielewa hili. Tajiri anaona ni rahisi kwenda Mwanza kwa kutumia ndege maana ataokoa muda mwingi sana maana haitachukua masaa mawili kufika Mwanza na kuweza kuendelea na shughuli zake. Hapo amepigania muda wake usipotee maana anahitaji muda zaidi kuliko pesa. Hivyo akilini mwake siku zote ni kuokoa muda si pesa, Na kama matokeo anaishia kuokoa muda na kutengeneza pesa Zaidi.
Natamani hili ulijue ikibidi hata kwa kukuchapa viboko maana kuna siri kubwa sana hapa.
Maoni
Chapisha Maoni